Kiswahili Form 3 Opener Term 1 Examination 2019
This file contains questions and the Marking scheme in it. Below is a preview of the questions
1. UFAHAMU (ALAMA 15)
Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata.
Macho ya Abdul yalipigwa na mwali mkali wa jua la asubuhi. Ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kuuona mwanga halisi wa ombwe lijiitalo dunia tangu alipohukumiwa kifungo gerezani. Punde tu komeo la mlango wa seli lilipofunguliwa, ilimIazimu Abdul ayafumbe macho kabla ya kuyafumbua tena taratibu ili yazoee mabadiliko yake.
Ilikuwa ndiyo siku ya Abdul ya kuachiliwa huru kutoka kwenye kifungo kirefu kilichoyapa macho yake mazoea ya giza la kaburi mle gerezeni. Macho yake yalipokwishaizoea ile hali na kumhakikishia kuwa kila alichokuwa akikiona si kizuka ila uhalisia, alipiga hatua. Akatoka nje ya mlango wa seli, kisha kwa kutoamini, akageuka nyuma kulitazama tena lile pango alimokuwa ametikwa katika muda huo wote. Akayafikicha macho kwa kutoamini huku machozi yakimdondoka asijue kama yalikuwa ya furaha au ya huzuni. Alipogeuka kuanza safari ya uhuru wake, macho yake yalikumbana na lango la gereza. Hapo, akasita kidogo, labda kuhakikisha kama kweli alikuwa huru. Bila shaka, hakuna askari wa gereza aliyemshikia bunduki au kumuamuru asimame. Walimtazama tu na kumpa tabasamu.
Taratibu, Abdul aliendelea kupiga hatua. Mhemko aliokuwa nao kutokana na hewa safi iliyompenya mapafuni uliufanya moyo wake upige kwa kasi. Ghafla, tabasamu ikapasua mashavuni pake. Akasita. Akaiinua pua yake iliyompa hakikisho kuwa uvundo na uozo wa seli haukuwa naye tena. Ingawa mwili wake uiijaa mabaka ya uchafu na matambara yaliyouficha uchi wake kuvunda, hilo halikumkera tena. Kwa hivyo, akatia tena tabasamu. Lake kuu lilikuwa shukrani kwa kuepuka yale madhila ya joto na rundo la wafungwa. Na kama hilo halikutosha, aligeuka tena ili sasa kuliangalia lile gereza. Bila kutarajia, alipiga magoti, akainua mikono kupiga dua, “Ewe Mungu, niepushe na balaa nyingine.”
Safari ya Abdul kutoka katika majengo ya gereza ilikumbwa na mseto wa mawazo. Alipokuwa katika ujia uliomwelekeza katika barabara kuu, mambo mengi yalimpitikia mawazoni asipate jawabu. Hakujua kama wazazi wake walikuwa wangali . hai, na kama walikuwa bado wanaishi katika nyumba ile ya kukodi kwa miaka hiyo kumi aliyokuwa jela, 'Je, nikiwakosa, nitaenda wapi? Nitaanzia wapi kuwatafuta?’ Mawazo hayo yaliifungua mifereji ya machozi, kisha ile ya makamasi, Balagha hiyo ilimfikisha katika kituo cha magari ya uchukuzi kwa ule aliouona kuwa muda wa kufumba na kufumbua. Aliyafuta.machozi yake haraka kwa kiganja kisha akaziba tundu la pua, tayari kupenga kamasi. Hata hivyo, kabla hajafanya hivyo, nafsi yake ilimtahadharisha kuwa hatua hiyo ingekatiza uhuru aliopewa kwa kuchafua mazingira. Kwa hivyo akaghairi. Akavuta ncha ya shati lake na kuitumia kama hankachifu kutimiza azma yake.
Hapo kituoni, matatu iliyokuwa mbele ilikuwa na watu wachache. Abdul akaingia na kukaa upande wa kioo ambapo tafakuri nyingi zilimjia. Akakumbuka jinsi kesi yake ilivyoendeshwa kinyume kabisa na ukweli na hukumu kutolewa kinyume cha haki. Mimi Abdul, mtoto twaa tangu kuzaliwa kwangu hata mdudu sijawahi kumponda kwa udole wangu, ndiyo sasa nije kusingiziwa kuua mtu? Mungu wangu! Kwa nini dunia hii haina wema? Kwa nini wanaodaiwa kuwa wasomi hata wakapewa jukumu la kuwakilisha maslahi ya raia ndio wanaowadhulumu hao raia? Hivi, hata hukimu na tajiriba yake aliamua kufuatilia zile porojo za wanaojiita majasusi? Angeahirisha hukumu yake ili kufanya uchunguzi zaidi, bila shaka nisingepata mapigo na dhuluma hizo zote. Kwa kweli, hii ni dunia ya mwenye nguvu mpishe!
Abdul alijisemea.
Maswali.
a. Je Abdul alikuwa gerezani kwa sababu gani? (alama 2)
b. Ni mambo yapi yaliyomtia Abdul tumbo joto alipowachiliwa huru. (alama 3)
c. Ukirejelea kifungu eleza mashaka katika asasi za kurekebisha tabia (alama 4)