Get premium membership and access revision papers with marking schemes, video lessons and live classes.

Kiswahili Paper 2 Form 3 End of Term 3 Examination 2019

Class: Form 3

Subject: Kiswahili

Level: High School

Exam Category: Form 3 End Term 3 Exams

Document Type: Pdf

    

Views: 1676     Downloads: 35

Exam Summary


Kiswahili Paper 2 Form 3 End of Term 3 Examination 2019
This file contains questions and the Marking scheme in it. Below is a preview of the questions


A. UFAHAMU (Alama 15)

Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuatia:
Shule yangu ya upili
Majio yangu katika shule hii ya upili hayakutokea kwa bahati nasibu bali kwa mipango kabambe niliyoianza tangu nikiwa shule ya vichekechea. Nikiwa sitetereki hata kwa wazazi wangu waliponisihi nijiunge na shule nyingine za karibu nikawa sisikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Nikawa na ragba ya mkanja nikingoja siku ya kujiunga na shule yenyewe. Kweli majuto ni mjukuu na huja kinyume.
Nilizaliwa katika aila yenye nafasi iliyotopea na kubobea katika ukwasi uliodhihirika kutokana na mitaa tulikoselelea kwa muda kabla ya baba kuaamua kununua nyumba yake mwenyewe huko upande wa Karen hivyo tukagura kutoka Runda. Wakati wa likizo tukawa tunaruka hadi pwani ambako mama yangu alikuwa amemiliki jumba lililokuwa katika ufuo wa bahari lililojengwa katika kipande kisichopungua ekari tatu alilotunukiwa wakati wa nikahi yao na wakwe wa baba yangu.
Wavyele wangu wakawa wanaendesha magari meusi ya kifahari ingawa sikuwahi kumwona mama akichangamka kuendesha magari yake ya maana, kila macheo ya siku za kazi gari lililoendeshwa na dereva ambaye alimstahi mama hadi akawa anamfungulia mlango wa gari na kuufunga baada ya mama kujitoma katika tumbo la gari lilimjia na kumrejesha kwa wakati. Nikajiunga na shule ya msingi ya kibinafsi ambako nilishughulikiwa kama kikembe. Wengi wa wale tuliosoma nao walikuwa wa tabaka langu na walikuwa wametoka katika kila sehemu nchini Kenya.
Hayawi hayawi huwa na siku ya kuripoti ikafika. Alfajiri, dereva mmoja akatumwa kwenda hadi Kisumu ili atulaki na kutusafirisha kutoka uwanja wa ndege hadi shule ya upili ambayo ilikuwa yangu ya rohoni. Nasi tukaelekea hadi uwanja wa ndege ili turuke hadi Kisumu. Safari yetu kutoka kitongoji cha kifahari hadi Airport ilikuwa njema, safari yetu tulipoabiri ndege ilikuwa bila bughudha, safari yetu kutoka Kisumu mjini haikuwa na kasoro na tulienda kulingana na mpango. Safari yetu ilikuwa mufti hadi tulipofika katika lango la shule ya kitaifa!
Tulipotia ozi tu!!....jamani......jamani nikafa moyo. Labda mama aliweza kubaini mabadiliko ya hisia zangu, nilitamauka, nikawa mchege na kusema kweli niliyoyaona sikuamini. Mvua iliyokuwa imepasua hapo awali ilikuwa imeacha vitua vya maji kwenye vijia vya kutembea vilivyochakaa na kubomoka bila yeyote kujali kuvikarabati. Majengo yalikuwa makongwe yaliyojengwa miaka mia moja iliyopita na yalistahili kuitwa makafadhi badala ya pahali pa kumkaribishia mwanafunzi aliyepita kwa alama mia nne na thelathini na tano.
Asiye na wake ana Mungu, nikapiga moyo konde lazima nisajiliwe katika shule ya ndoto langu. Ningewezaje kughairi wazo langu baada ya siku hizo zote za maandalizi tena mbele ya wanuna walioniona kama kielelezo chao tangu walipozaliwa. Nikasajiliwa!
Sikujua, hakika sikujua, sikujua shule ya upili ya kitaifa yaweza kuwa hivi. Kweli mwanafunzi aweza kukosa viatu na hata kushindwa kununua rangi ya kupaka viatu hivyo iwapo amenunuliwa na wahisani? Nilimlaumu ninamaana hakunieleza kuwa mtu anaweza kula chakula ambacho mbwa wetu hawezi hata kukiangalia. Nilipoingia katika ukumbi wa chakula nilihisi kitefutefu nusura nichafukwe na moyo, makapi ya mboga na uchafu usioelezeka ulinikumba, kisha nikapewa kisahani cha plastiki na kupakuliwa kipande cha ugali ambacho bado kilikuwa na unga na kuachiwa hiari ya kukila au kukitupa. Wenzangu wakawa wanakirambatia chakula kwa kasi huku mmoja wao alipoona jinsi nilivyokiangalia changu akanihisi nimpe chote na kukimaliza fyu. Wote walikuwa na furaha kemkem na kuajabia utukufu wa shule iliyotukuka ya kitaifa ila mimi.

Baada ya mlo ‘rojo rojo’, tukaelekea darasani nilikopigwa na mghuma mkubwa. Tulikuwa wanafunzi hamsini na watano katika darasa moja tu! Mwalimu mmoja akaja na kutukaribisha shuleni kisha akatuarifu kuwa atakuwa mwalimu wa darasa letu. Nilipomsikia akinena nusura niishiwe na stahamala, kimombo chake kilinishangaza, hasa matamshi yake yalipungukiwa na kudhirisha athari za lugha ya asili. Nilihisi kana kwamba ningemrekebisha lakini sikudhubutu.

Tukafululiza hadi bweni na nikajilaza kitandani chembamba huku mwingine nisiyemjua lakini asiyejua kuwa kuna nguo maalum za kulala akalala uchi katika ghorofa ya juu ya kitanda chetu. Mgeni njoo mwenyeji apone maana baada ya muda wadudu ambao sikuwahi kuwaona aushini mwangu wakanza kunishambulia. Nikaamka baada ya kumnasa mmoja wa wadudu hawa na kuuliza mmoja wa wenzangu ni wepi wadudu hawa na kwa kutojali hata kidogo, akanieleza kuwa hawana neno bali ni kunguni tu, sikujua na kwa kweli mama hakuniambia kuwa kuna wadudu wanaotafuna mtu na hunuka fye! Sikulala kwa hofu huku wenzangu wakiforota kwa njia ya kunighasi. Sikuwahi kudhani kuwa watu wengi wanaweza kulala chumba kimoja huku changu kikiwa na hamamu na vifaa vyote muhimu kikibaki bila mtu!
Tulisomeshwa na walimu wasiojali kana kwamba tunaelewa au la. Hawakushughulika iwapo tulifanya kazi za ziada au la, ndio, hakujali chochote. Kilichonishangaza ni kuwa wanafunzi waliojiunga nasi kutoka shule za umma wenye alama duni waliwapenda na kuelewa haraka walichosomeshwa na hawakujali matamshi yao, labda hawakuyatambua.
Hatimaye tukafanya mtihani wa mwisho wa muhula wa kwanza. Nilishangaa ghaya iliponibainikia kuwa aliyetuongoza alikuwa ghulamu mmoja mshamba niliyempuuza tu mvulana kutoka kijijini ambacho singetambua katika ramani ya nchi ambaye hata vitu vya kimsingi vilimpiga chenga. Nikafanya uchunguzi nikatambua mwenzangu alikuwa na alama mia mbili hamsini na tatu akitoka katika darasa la nane, nilifanikiwa kuwa nambari mia mbili hamsini na tatu kwa jumla ya wanafunzi mia tatu!
Tulipofunga kwa likizo ya Pasaka nikaamua kuchukua hatua nyingine sitawahi kuhama kutoka shule hii ya upili wala kuwa zaidi ya nambari kumi!

Maswali
a) Thibitisha kauli kuwa msimulizi ana msimamo dhabiti (alama 2)
b) Tofautisha jinsi mwandishi alivyofunzwa katika shule ya kibinafsi na shule ya upili. (alama 3)
c) Taja mambo matatu yanayotuonyesha kuwa msimulizi alilelewa katika aila ya kikabaila kulingana na aya ya pili.(alama 3)
d) Andika masuala matatu yaliyomshangaza katika shule ya upili (alama 3)
e) Andika tamathali mbili zilizotumika katika kifungu. (alama 2)

 

More Examination Papers